Home Uncategorized Rais mstaafu ajitoa chama Tawala

Rais mstaafu ajitoa chama Tawala

0
Obasanjo ajiengua chama tawala nchini Nigeria  
 Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ametangaza kujiengua kutoka
chama tawala cha nchi hiyo cha People’s Democratic (PDP). Hayo yanajiri
katika hali ambayo zimebakia wiki sita kuelekea uchaguzi mkuu wa nchi wa
rais. Jana mchana Obasanjo alitangaza kujiondoa rasmi katika chama
hicho, na kuichana hadharani kadi ya uanachama wake. Siku mbili kabla
rais huyo wa zamani wa Nigeria alitangaza kuwa, Rais Goodluck Jonathan,
anafanya njama za kila aina kuhakikisha anaendelea kubakia madarakani.
Olusegun Obasanjo mwenye umri wa miaka 77 na aliyewahi kuhudumu kama
jenerali jeshini, aliliongoza taifa la Nigeria mwaka 1970, na baada ya
nchi hiyo kurejea kwenye mfumo wa kidemokrasia mwaka 1999, akaiongoza
tena nchi hiyo kwa mihula miwili. Inaelezwa kwamba, uungaji mkono wa
Obasanjo kwa Jonathan ulipelekea rais huyo wa hivi sasa wa Nigeria
kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2011, hata hivyo uhusiano wa
wawili hao umeharibika katika miaka ya hivi karibuni. Aidha hivi
karibuni, Obasanjo alitangaza azma yake ya kumuunga mkono Muhammad
Buhari, mpinzani mkuu wa Jonathan katika uchaguzi wa tarehe 28 mwezi
Machi mwaka huu. Weledi wa mambo wameitaja hatua ya kujiondoka katika
chama tawala mwanasiasa mkubwa huyo kwamba itapelekea uchaguzi wa mwaka
huu, kuwa na mchuano mkubwa.
Facebook Comments